DC KAHAMA AKUMBUSHA WANAUME KUREJEA WAJIBU WA MALEZI YA WATOTO ILI KUPUNGUZA UKATILI

Mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyoandaliwa na Vituo vya Maendeleo ya Mtoto na Kijana Klasta ya Kahama.

Mkaguzi wa polisi Debora Kizanga akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyoandaliwa na Vituo vya Maendeleo ya Mtoto na Kijana Klasta ya Kahama.


Mkuu wa Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, Frank Nkinda, amewataka wanaume wilayani humo, kurejea katika wajibu wao wa malezi ya watoto ili kupambana na changamoto ya ukatili dhidi yao.


Amesema changamoto nyingi zinazoikabili jamii kwa sasa, ikiwemo ukatili dhidi ya watoto, mimba za utotoni, matumizi ya dawa za kulevya, kuongezeka kwa watoto wa mitaani na mmomonyoko wa maadili, zinachangiwa na kulegalega kwa malezi ndani ya familia hususani wanaume.


DC Nkinda ametoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, yaliyoandaliwa na Vituo vya Maendeleo ya Mtoto na Kijana Klasta ya Kahama.


Amesema serikali inaendelea kuweka sheria, sera na mifumo ya kulinda haki za watoto, lakini msingi wa malezi bora unabaki kuwa jukumu la wazazi, walezi, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla.


"Wanaume tunazaa sana, lakini jukumu la malezi tumeacha kwa akina mama, nao wanawaacha watoto kwa bibi zao. Serikali inaweza kuweka sheria lakini malezi ya mtoto huanzia nyumbani. Bila wazazi kutimiza wajibu wao tutazidi kuona changamoto nyingi katika jamii. Tuwalee kiroho pia.”


Amesema baadhi ya vijana wanaoshindwa kupata nyaraka muhimu kama vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho vya Taifa, kutokana na changamoto za kutowafahamu wazazi wao wa kiume, hali inayotokana na kukosekana kwa malezi na uwajibikaji wa wazazi.


"Leo ukienda maeneo mengi utakuta vijana wamejiingiza katika makundi yasiyo na mwelekeo. Vijana wanaachwa wanaenda kuishi magetoni na kujitegemea kabla ya umri lakini kibaya zaidi malezi ya chini huku hayakuwa mazuri,matokeo yake tunazalisha wahalifu.” Amesema Nkinda


Aidha Nkinda amewataka wazazi kuhakikisha watoto wao hawatumiki katika vitendo vya uvunjifu wa amani au kushawishiwa kushiriki vurugu zinazoweza kuhatarisha usalama wa jamii.


Amesisitiza kuwa Kahama itaendelea kulindwa ili kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi katika mazingira ya amani na utulivu.


Kwa upande wake, Mratibu wa Vituo vya Maendeleo ya Mtoto na Kijana Klasta ya Kahama, Renea Enos, amesema taasisi hiyo imeendelea kushirikiana na familia, shule, makanisa na wadau mbalimbali katika kuwajengea watoto na vijana mazingira bora ya ukuaji.


Amesema kwa sasa Klasta ya Kahama inahudumia zaidi ya watoto na vijana 1,200 kupitia programu mbalimbali za elimu, malezi, stadi za maisha, maendeleo ya kiroho na uwezeshaji wa kiuchumi kwa familia.


"Tunawahimiza watoto na vijana kujitambua kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii, kukua katika maadili mema, hofu ya Mungu na kujenga uwezo wa kujitegemea kiuchumi," Amesema Enos


Amesema zaidi ya vijana 120 wamepatiwa mafunzo ya stadi za maisha na ujuzi wa kujitegemea, huku wengine wakinufaika na michezo, sanaa na programu mbalimbali za kukuza vipaji.


Aidha, amesema zaidi ya vijana 30 wamefanikiwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu na kupata mikopo ya masomo kwa msaada wa shirika la Compassion linaloshirikiana na vituo hivyo.


Taasisi hiyo imekuwa ikiwapatia elimu ya malezi wazazi na walezi zaidi ya 600, ikiamini kuwa familia imara ndiyo msingi wa kuwa na watoto na vijana wenye maadili mema na mchango chanya katika maendeleo ya Taifa.


Hata hivyo amesema zipo changamoto zinazoendelea kuwakabili watoto na vijana ikiwa ni pamoja na mimba za utotoni, ndoa za utotoni, migogoro ya kifamilia, kuachana kwa wazazi na kukosekana kwa malezi ya karibu ya watoto, hali inayochangia baadhi ya watoto kuishi katika mazingira hatarishi au kukosa mwelekeo wa maisha.

Amesema "Changamoto nyingi zinazowakabili watoto leo zinatokana na migogoro ya kifamilia na kuyumba kwa malezi. Tukiimarisha familia, tutakuwa tumejenga misingi imara ya maendeleo ya mtoto na Taifa kwa ujumla.


Katika maadhimisho hayo, baadhi ya watoto akiwemo David William na Eliza Amos kutoka kituo cha huduma ya mtoto Kahama, wameiomba serikali kuzipitia upya na kuzipa nguvu sheria za ulinzi wa mtoto ili kuondoa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
















0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم