CHW KISHAPU WAJENGEWA UWEZO KUHUSU AFYA YA KINYWA NA MENO

Na Sumai Salum- Kishapu 

Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Julai 16,2016 wamepatiwa mafunzo kuhusu afya ya kinywa na meno yaliyofanyika katika ukumbi wa VETA Kishapu.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha Afya ya Kinywa na Meno, kwa kushirikiana na mdau wa afya Colgate Palmolive, yakilenga kuwajengea uwezo wahudumu hao ili waweze kutoa elimu sahihi ya afya ya kinywa na meno kwa wananchi katika jamii wanazozihudumia.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya kitengo cha kinywa na meno Dr. Ibrahimu Makongwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo amewasisistiza wahudumu hao wa afya ngazi ya jamii kuhakikisha wanayatumia mafunzo hayo kwa vitendo kwa lengo la kuisaidia jamii na ili kufikia malengo ya serikali kupitia Wizara hiyo na kuleta afya imara kwa wanachi.

Mratibu wa Afya ya Kinywa na Meno ngazi ya Mkoa, Nuruh Mpuya, akizungumza na wahudumu hao amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya afya na wadau mbalimbali katika kuimarisha huduma za kinga na elimu ya afya kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mratibu wa Afya ya Kinywa na Meno wilayani Kishapu, Anold Geminiani, amewawezesha washiriki kwa kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa kinga, usafi wa kinywa na meno, pamoja na njia bora za kuzuia magonjwa ya kinywa na meno.


Kwa upande wake, Mratibu wa Shirika la Colgate Palmolive, Christian Noah, amewahimiza wahudumu wa afya ngazi ya jamii kutumia maarifa waliyoyapata kuwafikia wananchi kwa kutoa elimu itakayosaidia kuboresha afya ya kinywa na meno katika jamii.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza uwezo wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika kuhamasisha tabia bora za usafi wa kinywa na meno, hatua ambayo itachangia kupunguza magonjwa ya kinywa na meno na kuboresha afya ya wananchi wa Wilaya ya Kishapu.






0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم