DIWANI SARA AIBUA HAMASA IDUKILO, AKABIDHI JEZI NA MIPIRA KWA BIASHARA UNITED

Diwani wa Kata ya Idukilo wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Sarah Marco, ameongeza hamasa katika sekta ya michezo baada ya kukabidhi jezi moja na mipira miwili kwa timu ya Biashara United ya Idukilo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono vijana wanaoshiriki mashindano ya Seso Cup.


Zoezi la makabidhiano limefanyika Agosti 7, 2026 katika viwanja vya Shule ya Msingi Idukilo, likishuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, ambapo Diwani huyo amesema ameamua kuunga mkono michezo kutokana na mwitikio mkubwa wa vijana katika mashindano hayo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhe. Sarah Marco amesema michezo ni moja ya njia muhimu ya kuwaweka vijana katika shughuli zenye manufaa, huku akieleza kuwa amefarijika kuona vijana wa Idukilo wakijitokeza kwa wingi na kuonyesha hamasa kubwa katika mashindano hayo.

“Tunaomba vijana wetu wawe bize na michezo. Tunajisikia faraja kuona wanajitokeza na wanaonekana kuthaminiwa. Michezo inaweza kuwa sehemu ya kujenga vipaji, umoja na kuwafanya vijana kutumia muda wao vizuri,” amesema Mhe. Sarah Marco.

Katika hatua nyingine, Mhe. Sarah Marco amesema amefarijika kuona timu ya Biashara United ikifanya vizuri katika mashindano hayo na ameahidi kuendelea kushirikiana na vijana katika kuhakikisha michezo inaendelea kukua katika Kata ya Idukilo.

Aidha, Diwani huyo ameeleza kuwa pamoja na msaada huo kwa Biashara United, amepanga pia kufikisha msaada kwa timu ya Lubaga FC ya Igumangobo iliyoko Kata hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Timu ya Biashara United, Kashinje Jilo, amemshukuru Diwani Sarah Marco kwa msaada huo na kuahidi kuwa vifaa hivyo vitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa huku akieleza kuwa timu hiyo bado inahitaji jezi na mipira zaidi ili kuimarisha maandalizi yake.

“Tuliomba tupate jezi moja na tumefanikiwa kuipata. Tunajisikia faraja sana kwa sababu tunaona vijana wetu wanathaminiwa. Tutaendelea kutumia vizuri vifaa hivi na tunaomba wadau wengine waendelee kutuunga mkono kwa jezi na mipira zaidi,” amesema Jilo.

Jilo amesema mwitikio wa vijana katika mashindano ya Seso Cup umekuwa mkubwa, huku hamasa ikiendelea kupanda kutokana na vijana kuitikia kwa wingi na kushiriki katika michezo hiyo ijapokuwa bado kuna baadhi ya vifaa vingine tungependa kuvipata pia vinavyohitajika katika kukuza michezo ikiwemo jezi nyingine moja au mbili za kuwa tunabadilisha, mipira, vifaa vya wakati wa mazoezi, gloves za golikipa.

Baada ya zoezi la makabidhiano, Mhe. Sarah Marco pamoja na Mhe. Peter Masindi walishuhudia mchezo wa hatua ya nusu fainali uliowakutanisha Biashara United na wapinzani wao, ambapo Biashara United ilifanikiwa kuicharaza bao 1-0, matokeo yaliyoiwezesha timu hiyo kutinga hatua inayofuata ya nusu fainali itakayochezwa.

Mashindano hayo ya Seso Cup yanafadhiliwa na Seso Ngalula, yakilenga kuwaunganisha vijana kupitia michezo, kukuza vipaji na kuwafanya vijana kutumia muda wao katika shughuli zenye tija huku yakitoa fursa kwa vipaji vya soka kuonekana na kuendelezwa.








0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم