DAS FATMA AHIMIZA JAMII KUUNGA MKONO UNYONYESHAJI, ASEMA NI MSINGI WA AFYA NA MAENDELEO YA MTOTO

Na Sumai Salum – Kishapu


Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga imefanya kilele cha maadhimisho ya 34 ya wiki ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama duniani huku Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Fatma Mohamed akiwa ndiye mgeni rasmi , akimwakilisha Mkuu wa Wilaya, ameziomba familia na jamii kwa ujumla kuendelea kuunga mkono unyonyeshaji wa maziwa ya mama, akisisitiza kuwa ni msingi muhimu wa kujenga kizazi chenye afya, akili na uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa.


Fatma amesema hayo Agosti 7, 2026 wakati wa maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Unyonyeshaji Duniani kiwilaya yaliyofanyika katika Kijiji cha Bubinza, Kata ya Mwamashele, ambapo amewataka Wanaume kuwapa wake zao ushirikiano wa kutosha kwa kupunguza mizigo isiyo ya lazima, kuwapatia lishe bora na kuwapa muda wa kutosha wa kunyonyesha watoto wao bila msongo wa mawazo.
Katibu Tawala wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Fatma Mohamed akizungumza wakati wa maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Unyonyeshaji Duniani kiwilaya yaliyofanyika katika Kijiji cha Bubinza, Kata ya Mwamasheleyalibeba kaulimbiu inayosisitiza kuwa "Mwanzo Imara wa Maisha ya Mtoto Uanza na Maziwa ya Mama," Agosti 7, 2026

"Unyonyeshaji wa maziwa ya mama si jukumu la mama pekee, bali ni wajibu wa familia nzima. Baba anapomsaidia mama kwa kazi za nyumbani, Mashambani, kumpa mapumziko na mazingira yenye utulivu, anakuwa amechangia moja kwa moja ukuaji bora wa mtoto. Serikali inaendelea kuhimiza ushiriki wa wanaume katika malezi kwa kuwa mtoto mwenye afya njema hujengwa na familia yenye mshikamano," amesema Fatma.


Aidha, amewahimiza wananchi kuzingatia elimu inayotolewa na wataalamu wa afya kuhusu unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza, kisha kuendelea kunyonyesha hadi mtoto afikishe miaka miwili huku akipewa vyakula vya nyongeza vinavyokidhi mahitaji ya lishe.
Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Furaha Kaburwa akizungumza wakati wa maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Unyonyeshaji Duniani kiwilaya yaliyofanyika katika Kijiji cha Bubinza, Kata ya Mwamasheleyalibeba kaulimbiu inayosisitiza kuwa "Mwanzo Imara wa Maisha ya Mtoto Uanza na Maziwa ya Mama," Agosti 7, 2026

Akitoa elimu ya lishe, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Furaha Kaburwa, amesema unyonyeshaji ni zawadi ya kudumu ambayo mama humkabidhi mtoto wake, akisisitiza kuwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo ndiyo msingi wa maisha imara ya mtoto. Amesema maziwa ya mama humkinga mtoto dhidi ya magonjwa, huchochea ukuaji wa mwili na ubongo, humjengea kinga ya mwili na kumpa lishe kamili inayohitajika katika hatua za awali za maisha.

Kuburwa amefafanua kuwa baadhi ya akina mama huingiwa na hofu pale mtoto anapolia wakidhani maziwa hayatoshi, jambo ambalo si sahihi wakati wote. Amesema mtoto anayekojoa mara sita hadi nane kwa siku, mwenye uzito unaoongezeka na anayetoa choo chenye rangi ya njano huonesha kuwa anapata maziwa ya kutosha. Pia amesisitiza kuwa mama hapaswi kukaa zaidi ya saa tatu bila kumnyonyesha mtoto kwa kuwa hali hiyo hupunguza uzalishaji wa maziwa.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Nourish kutoka Shirika la WorldVision Kishapu, Jackline Kawiche, amewataka akina mama kutokata tamaa wala kuwahi kuanza kumpa mtoto chakula kabla ya kufikisha miezi sita, akisema kufanya hivyo ni kumnyima mtoto haki ya lishe bora anayopaswa kuipata kupitia maziwa ya mama.
Meneja wa Mradi wa Nourish kutoka Shirika la WorldVision Kishapu, Jackline Kawiche  akizungumza wakati wa maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Unyonyeshaji Duniani kiwilaya yaliyofanyika katika Kijiji cha Bubinza, Kata ya Mwamasheleyalibeba kaulimbiu inayosisitiza kuwa "Mwanzo Imara wa Maisha ya Mtoto Uanza na Maziwa ya Mama," Agosti 7, 2026

Ameeleza kuwa msongo wa mawazo unaweza kupunguza uzalishaji wa maziwa, hivyo familia zinapaswa kuwapa akina mama mazingira ya utulivu na msaada wa karibu. Ameshauri kuwa mama anapopata changamoto hiyo apewe muda wa kupumzika, ahamasishwe kumweka mtoto karibu na kifua na kufanyiwa mguso wa taratibu sehemu ya mgongo ili kuchochea kurejea kwa maziwa.

"Naomba kina Baba niwape siri hii, wakati ambapo unaona mke wako amepata mawazo yoyote yatakayopelekea kupunguza kiasi cha uzalishaji wa maziwa kifuani mwake, ingia nae chumbani kisha anza kumchua eneo la mgongo hapa chini kidogo ya shing0 kwani utamrahisishia kurejesha mfumo wa uzalishaji maziwa kurudi kwenye hali yake ila kumbuka jambo kubwa zaidi tendo la kunyonyesha linahitaji utulivu sana" Ameongeza Kawiche.


Naye Diwani wa Kata ya Mwamashele, Mhe. Lukas Nkende, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kupeleka huduma za elimu ya lishe na afya katika maeneo ya Vijijini, akisema hatua hiyo imeongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji na malezi bora ya watoto huku akiwataka wananchi kutumia elimu wanayoipata katika utekelezaji.


Diwani wa Kata ya Mwamashele wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Lukas Nkende, akizungumza wakati wa maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Unyonyeshaji Duniani kiwilaya yaliyofanyika katika Kijiji cha Bubinza, Kata ya Mwamasheleyalibeba kaulimbiu inayosisitiza kuwa "Mwanzo Imara wa Maisha ya Mtoto Uanza na Maziwa ya Mama," Agosti 7, 2026

Baadhi ya wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo wamepongeza juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo Shirika la WordVision kufikisha elimu ya lishe na unyonyeshaji katika vijiji vya Wilaya ya Kishapu, wakisema elimu hiyo imewasaidia kubadili mitazamo kuhusu malezi ya watoto na kuwapa uelewa wa umuhimu wa maziwa ya mama katika kujenga mwanzo imara wa maisha ya mtoto.


Maadhimisho hayo yalibeba kaulimbiu inayosisitiza kuwa "Mwanzo Imara wa Maisha ya Mtoto Uanza na Maziwa ya Mama," huku wataalamu wa afya wakikumbusha kuwa maziwa ya mama ni zaidi ya chakula, ni kinga, afya na msingi wa maendeleo ya mtoto na taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Bubinza kilichoko Kata ya Mwamashele wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Sheni Shimba
Mwenyekiti wa Kijiji cha Lwagalalo kilichoko Kata ya Mwamashele wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Sali Mwandu Dutu(wa kwanza kushoto)

















































































0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم